12 Mei 2023 - 14:37
Interpol yataka kutambuliwa wanawake waliouawa katika nchi 3 za Ulaya

Polisi ya Kimataifa (Interpol) imeanzisha oparesheni iliyopewa jina la " Nitambue" ili kuweza kupata mabaki ya miili ya wanawake 22 waliouliwa katika nchi za Uholanzi, Ubelgiji na Ujerumani.

Idadi ya watu waliotoweka nje ya mipaka ya nchi zao imeongezeka katika miaka ya karibuni ikiwa ni matokeo ya kuongezeka wahajiri kimataifa na kushtadi vitendo vya uhalifu vya magenge ya magendo ya binadamu duniani. Wanawake ndio waathiriwa  wakubwa zaidi wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ukandamizaji wanaokumbana nao majumbani, kubakwa na magendo ya binadamu.  

Ripoti ya Euro News inaeleza kuwa, baadhi ya mabaki ya miili ya wahanga wa mauaji hayo yanayotajwa kufanyika huko Uholanzi, Ubelgiji na Ujerumani ambayo Interpol ilianza kuyachunguza kwa muda sasa, yamegunduliwa miaka kadhaa iliyopita. Imekuwa vigumu kutambua utambulisho wa wahanga wa mauaji hayo huku kukiwa na tetesi kwamba upo uwezekano kwamba waliouawa walikuwa raia wa nchi nyingine.  

Tathmini za awali zinaonyesha kuwa baadhi ya wanawake waliouawa walitoka katika maeneo fulani ya Ulaya Mashariki na katika upande mwingine,  tetesi zinaendelea kutolewa kuhusu utambulisho halisi wa wahanga hao. 

Kwa msingi huo, Polisi ya Kimataifa (Interpol) imeanzisha uchunguzi ili kutambua utambulisho wa wahanga wa mauaji hayo na hatimaye kuweza kuwatia nguvuni washukiwa wa jinai hiyo. Wakati huo huo waigizaji, waimbaji na wanariadha wa kike wamesambaza video na kuwatolea wito raia wa nchi mbalimbali kutaja majina ya wanawake hao waliouawa huko Uholanzi, Ubelgiji na Ujerumani. 

342/